NI nadra sana mwezi kwisha bila kusikia mwanafunzi amegongwa na gari ama pikipiki na kufariki alipokuwa akijaribu kuvuka barabara.Mara kadhaa nimewahi kuona ama kuelezwa na watu walioshuhudia ajali husika juu ya mazingira yaliyosababisha ajali hiyo. Watoto wengi wanaogongwa ni wale wanafunzi ambao unakuta wanavushwa barabara na wasichana wa kazi.Wengi utakuta wapo na kaka ama dada zao ambao kimsingi hawapishani sana kiumri.
Katika mazingira haya utakuta mtoto anamponyoka anayemwongoza na kurudi nyuma ama kukimbia mbele na mwisho hugongwa na gari ama chombo chochote kinachokuwa karibu.
Ukijaribu kuangalia, laiti kama mtoto huyo angekuwa na mtu mzima na aliye makini, kwa kiasi kikubwa ajali ingeweza kuepukika. Nasema mtu mzima na aliye makini kwa sababu, wakati mwingine msichana wa kazi anayepewa mtoto amvushe barabara, yeye mwenyewe anahitaji mtu wa kumvusha kutokana na ugeni wake kwenye mji mkubwa kama wa Dar es Salaam. Cha ajabu wazazi hilo hatulioni, unakaa nyumbani unamwagiza msichana wa kazi ampeleke mtoto wako kituoni ama shuleni, ukisikia amegongwa na kupoteza maisha utamlaumu nani?
Jambo la kufanya hapa ni lazima wazazi tuamke, tujue kuwa mtu wa kwanza anayeweza kumwangalia mtoto wako kwa makini ni wewe mwenyewe, hakuna mwingine. Msichana wa kazi akusaidie tu pale inapobidi, siyo kila jambo hata lile ambalo linahusu uhai wa mtoto wako. Wakati mwingine unakuta unategemea mtoto wa darasa la pili au la tatu amwongoze mtoto wa darasa la kwanza, Kwa hakika mzazi huyu hayuko makini. Watoto hawa wote bado vichwa vyao havipo tayari kwa kufanya uamuzi mgumu, lazima wawe na mtu mzima anayewaongoza barabarani.Tumeona watu wazima wakigongwa na kupoteza maisha, sembuse watoto wadogo.
Wakati mwingine tunatarajia kuwa watavushwa barabara na watu wazima watakaokutana nao huko njiani, hivi kuna watu wamewekwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo? Unawaamini vipi hao watu, ni vema mzazi ukahakikisha kuwa usalama wa mtoto wako unausimamia wewe mwenyewe, hata siku moja usimtegemee mtu mwingine.
NIMEIONA HII MAKALA ILIOANDIKA NA FERDY AZZAH UKO MWANANCHI NA NIKAONA NISHEE NA WASOMAJI WANGU, KWANI WENGI WAO NI WAZAZI NA TUNAHITAJI ZE WEKI UP CALL KUSISITIZA USALAMA WA WATOTO WETU WAENDAPO SHULENI MAANA SIKU HIZI AJALI ZIMEZIDI...
Chanzo cha habari: Mwananchi na Fredy Azzah
0 comments:
Post a Comment