Home » » HAUZGEL AUA MTOTO WA MIEZI 7

HAUZGEL AUA MTOTO WA MIEZI 7

Mtoto mwenye umri wa miezi saba, Anjela David, anadaiwa kuuawa na mfanyakazi wa ndani 

Mtoto mwenye umri wa miezi saba, Anjela David, anadaiwa kuuawa na mfanyakazi wa ndani jijini Dar es Salaam na kisha kutoroka na mizigo yake. Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, baba mzazi wa mtoto huyo, David Salakana, mkazi wa Sinza Afrika Sana alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, ingawa hana uhakika na muda kamili kitendo hicho kilipofanyika. Alisema kuwa juzi majira ya asubuhi aliondoka na mkewe kwenda katika shughuli zao na kumuacha mtoto wao akiwa na mfanyakazi huyo aliyemtaja kwa jina moja la Marietha (19). Salakana alisema mkewe, Anna Haule, ilipofika majira ya mchana alimpigia simu mfanyakazi huyo ili kufahamu hali ya mtoto wao kama tayari ameshampatia chakula au la. Alieleza kuwa mfanyakazi huyo baada ya kupigiwa simu hiyo alijibu kuwa haelewi kama mtoto huyo amekula au la na kwamba yeye (Marietha) hayupo ameondoka zake.


Alisema baada ya kumjibu hivyo, mkewe aliamua kumpigia simu kijana mmoja ambaye alimtaja kwa jina moja la Ally ambaye ni jirani yake na kumuomba aende nyumbani kwake na aingie ndani na kumuangalia mtoto huyo. Salakana alisema kijana huyo baada ya kufika alimkuta mtoto huyo akiwa amelala na alipojaribu kumuamsha hakuamka ndipo alipomueleza mkewe kuhusiana na hali hiyo. Hata hivyo, Salakana alisema baada ya mkewe kupatiwa taarifa hizo alirudi nyumbani ghafla na ndipo alipoamua kumchukua mtoto wao na kumpeleka katika Hospitali ya Marie Stopes iliyoko Sinza ili kumuangalia kama ni mzima au la na ndipo alipojulishwa kuwa alishafariki dunia. “Kutokana na mazingira hayo, nashindwa kukueleza kuwa mwanangu amefariki muda gani kwani muda ya mchana ndipo niliporudi na kumchukua na kumpeleka hospitali, sijaelewa vizuri kifo cha mwanangu kwani tulimuacha akiwa ni mzima halafu namkuta ni marehemu cha ajabu mfanyakazi katoroka na mizigo yake,” alisema Salakana.


Salakana alisema wakati anaingia chumbani alikuta chakula aina ya mtori kipo chini. "Sasa sijaelewa kama alimlisha mtoto chakula au la,” alisema. Alisema tayari amekwisha kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Kijitonyama, lakini mfanyakazi huyo ambaye anatokea Mkoa wa Shinyanga hajapatikana. Alisema mfanyakazi huyo baada ya tukio hilo, alifunga mizigo yake yote na kuamua kuondoka nyumbani hapo na kuelekea kusikojulikana huku simu yake ya kiganjani ikiendelea kuita bila kupokelewa. 


Soma habari kamili kwenye gazeti la: NIPASHE
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Sweet Home - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger