Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt (nyuma) akiwa amekwama kwenye lifti ya jengo la Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam jana, alipokwenda kumtembelea Waziri wa wizara hiyo, Prof Sospeter Muhongo. Picha ndogo watu waliokuwemo kwenye lifti hiyo wakijalibu kufungua kwa mkono baada ya kukwama
BALOZI wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt jana alikwama ndani ya lifti katika Jengo la Wizara ya Nishati na Madini, Dar es Salaam kwa takriban dakika 20.
Balozi Lenhardt akiwa na ujumbe wake wa watu wawili, walikumbwa na mkasa huo mchana wakati wakienda kukutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Mbali na Balozi Lenhardt na ujumbe wake, pia kulikuwamo na watu wengine wakiwemo maofisa wa wizara hiyo na kufanya jumla ya watu saba kukwama kwenye lifti hiyo.
Saa 7:58 mchana mwandishi wetu alipofika wizarani hapo, alimkuta balozi huyo na wenzake hao wakiwa wamekwama ndani ya lifti hiyo katika ghorofa ya kwanza huku ofisa wa mapokezi wizarani hapo akihangaika kufanya mawasiliano na mafundi.
Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo alifanikiwa kuifungua na kuacha uwazi wa kama sentimita 10 na kisha kuweka kibao ambacho kiliifanya iwe wazi lakini bila ya kuwawezesha waliokuwamo ndani kutoka. Hatua hiyo iliwawezesha Balozi huyo na wenzake walau kupata hewa wakati wakisubiri hatua zaidi za kuwakwamua. walibaki humo hadi ilipotimu saa 8:14 mchana walipokwamuliwa baada ya mafundi waliokuwa wamefika muda mfupi kabla, kufanikiwa kuifungua.
Kutokana na tukio hilo, mkutano wa Balozi huyo na Waziri Profesa Muhongo uliokuwa umepangwa kuanza saa 8:00 ulichelewa kwa zaidi ya nusu saa kusubiri wageni hao wakwamuliwe. Ingawa hakuna ofisa wa wizara hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia mkasa huo wa kukwama kwa lifti hiyo, ilielezwa kwamba tatizo hilo limetokana na lifti hiyo kuwa mbovu.
Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo ambaye hata hivyo, jina lake halikuweza kupatikana mara moja alisikika akisema kuwa lifti hiyo ina kawaida ya kukwama.
Baada ya kufanikiwa kutoka, Balozi huyo na maofisa aliokuwa ameambatana nao pamoja na maofisa wengine wa wizara waliingia katika chumba cha mkutano na kuendelea na mazungumzo. Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Waziri Profesa Muhongo alimtaka radhi Balozi Lenhardt na ujumbe wake kwa tukio hilo lakini akamtania kuwa bila shaka amepata uzoefu wa tatizo la nishati nchini, maelezo ambayo Balozi huyo aliyeitikia huku akicheka.
Mweeh aibuje..???
Habari na James Magai
Picha na Michael Jamson
Source : Mwananchi
2 comments:
uuuh jamani tz aibu kweli
uwii jaman aibu gani hiii mweee mweee hv hizi lifti zinafanyiwaga matengenezo kweli mungu wangu jengo lenyewe lile lilivyochoka khaaa kwa kweli ni aibu ya mwaka
Post a Comment